Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza Bibi Maligo Daimon baada ya kukabidhiwa Nyumba ya kuishi na Chakula na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Tulia Trust ambayo Mkurugenzi wake ni Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson, makabidhiano hayo yamefanyika katika Mata wa Ilolo jijini Mbeya, Mei 11, 2024.
SERIKALI imeanza mchakato wa ujenzi wa kituo jumuishi cha huduma za parachichi ambacho kitasaidia kuhifadhi na kuchakata zao la Parachichi kitakachojengwa eneo la Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.

Akizungumza baada ya Waziri Mkuu Kassim majaliwa ambaye yuko ziarani Mkoani Mbeya kuhoji kuhusu changamoto ya kuharibika kwa parachichi za wakulima katika eneo hilo, Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Enock Nyasebwa amesema kuwa wako katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kimkataba ili kumuwezesha mkandarasi kuanza ujenzi.

Ameyasema hayo jana (Jumamosi Mei 11, 2024) katika mkutano wa hazara wa Waziri Mkuu uliofanyika Kiwira wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

"Ujenzi wa kiwanda hiki utawezesha kuongeza thamani ya zao la parachichi kwani itawezesha wakulima kuhifadhi mazao yao katika chumba baridi pamoja na kuchakata mazao yatokanayo na matunda hayo ikiwemo mafuta".

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa katika kuhakikisha wanaongeza zaidi thamani ya zao hilo, wameanza mpqngo wa kuweka vugezo ili kuhakikiwha miche inayopandwa inakiadhi vigezo lengo likiwa ni kupata zao lenye ubora ambayo litafanya vizuri kwenye soko la kimataifa ili kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi huyo kuhakikisha wanakamilisha taratibu zilizobaki ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu kilimo bora cha zao la parachichi ili kuongeza thamani na ubora.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Busokelo lililoko eneo la Lwangwa na kuweka jiwe la msingi kwenye jengo hilo.

Mapema, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busokelo, Bi. Loema Peter alimweleza Waziri Mkuu kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 94 na akaomba Serikali ikamilishe taratibu za upatikanaji wa sh. bilioni 2.3 ili waweze kukamilisha hatua iliyobakia.

Alisema hadi hadi sasa wamekwishapokea shilingi bilioni 6.08 za ujenzi na shilingi milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa samani za ofisi hizo.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema michezo ni zaidi ya afya na burudani, ni fursa ya ajira na pia hupunguza magonjwa mwilini.

“Kama mnavyofahamu, michezo ni zaidi ya afya na burudani lakini leo tunathibitisha kuwa baada ya mbio hizi, sote tumefurahi na miili yetu imeimarika.”

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Mei 11, 2024) wakati akizungumza na viongozi, wananchi na washiriki waliohudhuria hafla ya kufunga hafla ya TULIA MARATHON iliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Amesema kwa mujibu wa Wizara ya Afya, michezo inawezesha watu kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. “Taarifa za Wizara zinasema kuwa nchi yetu inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, kiharusi na maumivu ya viungo kama magoti na mgongo. Kwa hiyo tujenge tabia ya kufanya mazoezi, ” amesema.

Amesema hivi sasa fedha nyingi zinatumika kutibu maginjwa hayo iwe ni kwa Serikali au mtu mmoja mmoja na kwamba magonjwa hayo yanaendelea kupoteza nguvukazi ya Taifa.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha michezo na hivyo kuongeza hamasa ya kitaifa ya kupenda michezo. “Sote tunakumbuka kuwa alianzisha mpango wa goli la Mama, akaanzisha changizo la Kitaifa kwa ajili ya timu za Kitaifa na hii inaenda sambamba na michezo ijayo ya AFCON 2027.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii izitumie mbio za Tulia Marathon kutangaza utalii wa mkoa wa Mbeya na mikoa iliyo jirani. “Mkoa huu una vivutio vingi na mikoa ya jirani inavyo vivutio mbalimbali. Tumieni mbio hizi kuwa fursa ya kutangaza utalii. TANAPA wekeni banda hapa, onesheni kuna vivutio gani kwenye mkoa huu na mikoa ya jirani,” amesema.




Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
-Rais Samia atunukiwa Tuzo ya Ubinadamu;

-Ombi la ruzuku kwa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania lafanyiwa kazi;

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Redcross Society) katika utoaji huduma mbalimbali za kibinadamu hususan nyakati za dharura.

Dkt. Biteko amesema hayo leo (Mei 11, 2024) Jijini Dodoma alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgemi rasmi katika maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania ambapo amesema huduma zinazotolewa na chama hicho zinazingatia sheria na kanuni na taratibu za kuanzishwa kwa chama hicho ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bila upendeleo.

‘‘Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kukiwezesha chama hiki kwa namna mbalimbali,…ombi lenu la Serikali kuwapatia ruzuku katika shughuli muhimu za jamii yetu tumelipokea na tunalifanyia kazi. Hadi sasa kuna ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa Chama cha Msalaba Mwekundu na viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali. Kila tunapofanya ziara tunashirikiana na nawaona kwenye shughuli za Serikali iwe sherehe, misiba ya kitaifa mkitoa huduma ya kwanza kwa washiriki, wakati wa majanga mbali mbali tunawashuhudia mkitoa huduma’’, amebainisha Dkt. Biteko.

Ametaja baadhi ya huduma zinatolewa katika nyakati mbalimbali ‘‘Chama hiki kimekuwa kikitoa huduma ya kwanza kwenye majanga mbalimbali yaliyotokea kama vile mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyotokea Hanang - Katesh, kuimarisha huduma za afya kwa kujenga wodi za wazazi na wodi za watoto na kina mama na kutoa vitendanishi, vifaa kinga na vifaa tiba, pamoja na kushiriki katika utoaji wa huduma za afya katika makambi ya wakimbizi’’, amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza ‘‘Serikali pia inatambua na kuthamini ushiriki wenu mkubwa mlioonesha kwenye maporomoko ya udongo yaliyotokea katika mlima wa Hanang – Katesh na juhudi zinazoendelea hivi sasa za kuisaidia Serikali kujenga nyumba 35 kati ya nyumba 101 za wahanga wa maporomoko hayo kama alivyoagiza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan’’.

Kufuatia jitihada za Chama cha Msalaba Mwekundu nchini ambacho ni kielelezo cha utu na ukarimu kwa binadamu, vile vile ni ishara ya uzalendo mkubwa, Desemba 12, 2023 Rais Dkt. Samia alitoa cheti cha kuwapongeza kwa kutambua mchango wao katika kushughulikia maafa ya mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewahimiza watanzania kuendelea kuiombea nchi kipindi hiki kuelekea Uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 waendelee kuiombea Tanzania ili uchaguzi huo ufanyike kwa Amani na usalama.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Red Cross Tanzania katika kuwasaidia wananchi wanaokumbwa na changamoto mbalimbali za majanga ambayo yamekua yakitokea kutokana na mabadiliko ya tabia nchi au kwa namna yeyote ile na kuwa viongozi wa umma wanapaswa kuwahudumia wananchi kwa furaha.

"Watanzania tumekuwa na moyo wa kujitoa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere Tanzania ilipopata uhuru ilijitoa kusaidia mataifa mengine, viongozi lazima kujitoa katika kufanya huduma na kazi zilizo mbele yetu kwa Watanzania milioni 61 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, tutoe uwezo wetu na nguvu zetu zote kuwasaidia", amesema Balozi Chana.

Naye, Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihanzile ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana nao na kuimarisha huduma mbalimbali nchini mfano kwa kujenga hospitali, shule na barabara.

"Mtoto akikosa tiba amepungukiwa huduma za kibinadamu, akikosa shuleni tunatakiwa tumsaidie, majanga kama maafa yanapoongezeka kwetu tunahusika, njaa au upungufu wa damu unapotokea ni jukumu letu kusaidia, ukimpata kiongozi ambaye mipango na maono yake inakwenda kupunguza haya, basi anawapunguzia kazi”, amesema Mhe. Kihanzile.

Amefafanua “Baada ya miaka zaidi ya 40 Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kinamkabidhi tuzo maalum kwa mtu mmoja tu, tuzo ya ubinadamu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni kutambua na kuheshimu mchango wake".

Mwakilishi wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Uganda, Bw. Halid Kirunda amesema kuwa nchi za Afrika Mashariki zimekua zikishirikiana katika shughuli za utoaji huduma za maokozi kwa kuzingatia sheria za haki za binadamu zinavyoelekeza kwakua ni kiunganishi baina ya wananchi na Serikali.

Sambamba na mafanikio mbalimbali aliyoyataja ambayo yamechangiwa na Chama hicho ameziomba Serikali kuendelea uwezeshaji wa fedha na vifaa vya shughuli za uokozi kwa kuwa baadhi ya vyama hivyo vinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha za kutosha na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uokozi.

Ameongeza kuwa msingi wa Chama cha Msalaba Mwekundu ni kutoa huduma za uokozi bure bila kubagua maeneo yakufika kwa vile wanatanguliza utu mbele na kazi hiyo wanaifanya kwa kujitolea hivyo ni vyema kuwasaidia watoa huduma hao kumaliza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ambazo zinawapa ugumu wakutekeleza majukumu yao.




Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kuandaa mfumo mmoja wa ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara nchini ili kuondoa kero ya taasisi mbalimbali za Serikali kukusanya kodi.

Alitoa kauli hiyo Mei 10, 2024 jijini Mbeya wakati wa Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta umma na Sekta binafsi uliokuwa na lengo la kujadiliana namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara katika Mkoa huo.

Aidha. Dkt. Kijaji alisema kero hiyo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali kuwa ilikuwa ikichangia kuua biashara na kufukuza wajasiriamali.

“Kilio hiki tumeshakisikia na kama Serikali tunaendelea na majadiliano ya kuanzisha mfumo mmoja wa kukusanya mapato, yatakusanywa kwenye kapu moja kisha kila taasisi itapata mgawo wake na hivyo kupunguza usumbufu,” alisema Dkt. Kijaji.

Aidha alisema Serikali za Tanzania na Marekani zimeanzisha chemba moja ya wafanyabiashara nchini marekani kwa lengo la kurahisisha ushirikiano wa biashara na kupunguza mlolongo wa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Vilevile aliwataka watanzania kuwa waaminifu kwenye biashara ili kuepuka kuharibu masoko ya kimataifa akidai kuwa fursa hiyo ya soko la marekani ni muhimu kulindwa pamoja na masoko mengine ya kimataifa.

Alisema wizara inaendelea na mazungumzo na Shirika la Ndege la Uturuki kwa ajili ya kuanza usafirishaji wa maparachichi yanayozalishwa nchini kwenda uturuki ambako kuna soko kubwa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah alisema Wizara hiyo imekuwa ikishirikiana na vyombo mbalimbali kufanya oparesheni za kukamata bidhaa bandia zinazoingizwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani na afya za wananchi.

Alisema hivi karibuni walifanya ukaguzi kwenye mikoa mbalimbali nchini na kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara wakiuza simu feki na hivyo wakachukua hatua za kisheria ikiwemo kutaifisha bidhaa hizo na kuwasweka ndani wahusika.

Aliagiza taasisi zinazohusika na usimamizi wa ubora wa bidhaa nchini kuendelea kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka ili kukuza viwanda vya ndani na kulinda usalama wa wananchi.

“Hatuwezi kuacha watu wanaingiza bidhaa feki nchini, bidhaa hizo ni hatari kwa Uchumi wetu na kwa maisha ya wananchi, kwahiyo niwahakikishie kwamba tutaendelea kuchukua hatua maana usalama wa watanzania upo mikononi mwetu,” alisema Abdallah.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chemba ya wafanyabiashara, viwanda na kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mbeya, Erick Sichinga alisema utitiri wa kodi umekuwa ukisababisha kutoelewana kati ya wafanyabiashara na taasisi za serikali.

Alisema baadhi ya taasisi zinazokusanya kodi na tozo zimekuwa zikifanya kazi bila kuwashirikisha watu wa sekta binafsi ili na wao watoe maoni yao hali ambayo inaendelea kusababisha migogoro.

Alisema moja kati ya taasisi ambazo zimekuwa zikiwakwamisha wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Taasisi ya Afya na Usalama mahali pa kazi (OSHA) ambazo zimekuwa zikiwatoza tozo kubwa.

Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Victoria Michael alisema baadhi ya Halmashauri na mikoa nchini imekuwa ikianzisha tozo mbalimbali ambazo zinakinzana na Mpango wa Kuboresha Mazingira ya biashara (MKUMBI).

Alisema lengo la mpango huo ni kutatua kero za kibiashara zinazowakumba wafanyabiashara lakini zinapoanzishwa tuzo mpya kwenye halmashauri ni uzalishaji wa matatizo mapya kinyume na lengo.

Victoria ambaye ni mchambuzi wa sera alisema sekta binafsi kwa sasa inachangia asilimia 50 na sekta ya umma inachangia asilimia 50 kwenye majadiliano ya kuboroesha mazingira ya biashara.

Ofisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Songwe, Elijah Simbeye alishauri serikali kutatua kero za kodi ikiwemo kuondoa utitiri wa kodi kwa kuziweka kwenye kapu moja ili kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara.









Dar es Salaam, 11 Mei 2024

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inaujulisha umma kuwa taarifa inayosambaa kuhusu ndege yake aina ya Boeing 787- 8 yenye usajili wa namba 5H-TCJ kupelekwa kwenye matengenezo makubwa yaani Check - C kabla ya kufikisha muda wake tangu inunuliwe na kutelekezwa nchini Malaysia sio za kweli.

Ndege yake ya B787- 8 ipo nchini Malaysia kwa ajili ya matengenezo ya lazima ya injini zake baada ya kufikisha muda wake na sio matengenezo makubwa ya Check - C.

“Matengenezo makubwa ya ndege zetu za 787 – 8 (Dreamliner) yanafanyika hapa nchini kwenye Karakana yetu ya KIMAFA iliyopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kila baada ya miaka 3 au masaa 12,000 chochote kitakachoanza. Karakana zetu zina wataalam wenye uzoefu wa kufanya matengenezo makubwa ya ndege ya kiwango cha Check – C”, amesema Mha. Matindi.

Ameongeza kuwa tangu ndege hizi ziwasili nchini zimefanyiwa matengenezo makubwa (Check - C) mara moja ambapo kwa ndege ya kwanza iliyowasili nchini mwaka 2018 ilifanyiwa matengenezo hayo mwaka 2021 na ya pili iliyowasili mwaka 2019 ilifanyiwa matengenezo mwaka 2022, amehitimisha, Mha. Matindi.

Tatizo la ndege kukaa muda mrefu kwenye karakana, Malaysia, linatokana na uhaba wa injini za ziada ambazo zingeweza kutumika wakati injini zake zikifanyiwa matengenezo.

Ndege za Boeing 787- 8 za ATCL zinatumia injini za Kampuni ya Rolls Royce aina ya Trent 1000. Kwa mujibu wa miongozo ya Mamlaka za Usafiri wa Anga na watengenezaji wa injini hizo, imekuwa ni lazima injini hizo kufanyiwa matengenezo makubwa (overhaul) kila baada ya miruko 1,000. Hii ni baada ya kugundulika kwa matatizo ya kisanifu (design) katika mifumo hasa ya ufuaji wa nguvu za kuendesha ndege, kwa injini nyingi za matoleo mapya. Aidha, Matatizo haya yamesababisha kutolewa kwa miongozo maalum kuhusu uchunguzi wa injini wa mara kwa mara iwapo katika matumizi.

Injini hizo zinapopelekwa kwa matengenezo zinalazimika kuzingatia foleni au zamu (slot) kutokana na idadi kubwa ya injini zinazosubiria matengenezo na hivyo kupelekea kuchukua muda mrefu kuhitimisha matengenezo yake. Kukosekana kwa injini za ziada kunasababisha ndege isubiri hapo karakana hadi kukamilika kwa matengenezo tajwa.

Kwa sasa matengenezo ya injini za ndege yetu iliyoko Malaysia tayari yanaendelea na inatarajiwa kurejea nchini mwanzoni mwa mwezi Juni 2024.

Imetolewa na:

Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma






Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa Msama Promotion, Alex Msama amewaomba Watanzania kukumbuka na kuenzi mambo mema yaliyofanywa na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Mbunge wa Mtama hayati Benard Membe wakati wa uhai wake.

Pia amewaomba kuendelea kuyasimamia yale yote mema ambayo Membe enzi za uhai wake alikuwa anataka yatekelezwe.

Akizungumza katika Misa ya Kumkumbuka Hayati Benard Membe iliyofanyika Kanisa la St. Joseph jijini Dar es Salaam Msama amesema Hayati Membe ameacha alama ndani ya Serikali katika nafasi mbalimbali alizotumikia ikiwemo ya Waziri wa Mambo ya nje, kwani matunda na alama aliyoicha inaigusa nchi.

Amesema wakati kesho Membe anatimiza mwaka mmoja tangu afariki dunia,Msama amesema kuna mambo mengi amefanya katika Taifa letu na kuna mengine aliyoawaachia Watanzania ili wayaendeleze.

"Kikubwa ambacho Hayati Membe ametuachia sisi watu wake wa karibu, tuwe wamoja, tusameheahane tunapokoseana...tusiwe watu wa kuzungumziana mambo yasiyosahihi .Pia tuwe wazalendo katika Taifa letu la Tanzania ili tuweze kuwasaidia na wengine ambao wanatakiwa kuinuliwa,"amesema Msama.

Ameongeza Watanzania wasisahau kumcha Mungu,wajitolee katika kazi za Mungu."Tuwe  tunasaidia miradi ya kazi za Mungu kwa lengo la kufanikisha kazi za Mungu zinasonga mbele. Sisi watu wake wa karibu na Hayati Membe, tunaendelea kuyaenzi yale ambayo yanatakiwa kuyafanya”




Kwa upande wake Waziri wa Habari , Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema wamekuwa na siku nzuri ya kutafakari kazi nyingi alizozifanya Hayati Membe nchini, hasa katika jimbo la Mtama alikozaliwa.

Amefafanua kuwa katika kumuenzi Membe wameandaa Misa ya kumkumbuka na kumuombea kwa Mungu."Kesho kaka yetu Benard Membe anatamiza mwaka mmoja tangu alipofariki Dunia.Tumekuwa na siku nzuri ya kutafakari kazi nyingi alizozifanya katika nchi yetu, katika jimbo la Mtama."

Akieleza zaidi Waziri Nape amesema kuwa katika Jimbo la Mtama, Hayati Membe alikuwa ni muumini wa kubadilisha maisha ya watu kwani wakati wa uongozi wake alikuwa akitamani kila mtu awe na maisha mazuri.

Amefafanua Hayati Membe alitamani  mtu aishi kwenye nyumba nzuri, apate maji safi, na hizo ndizo ndoto ambazo ameendelea nazo."Ndio maana tangu aliponiacha tumehakikisha tumesambaza umeme katika Jimbo letu.

"Tumepeleka maji kila mahali, mawasiliano, shule, na katika Kijiji na Kata aliyotoka wakati anaondoka hakukuwa na sekondari, hivyo tumejenga sekondari na tukaipa jina lake Benard Membe ili kumkumbuka."



 Katika kukabiliana na ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, kampuni ya Heineken Tanzania imeanzisha ushirikiano wa kimkakati na shirika la mazingira la Lead Foundation. Lengo la ushirikiano huu ni kufanya mipango endelevu ya kurejesha misitu iliyoharibiwa na kulinda mazingira yetu.


Meneja wa Kampuni ya Heineken Tanzania, Obabiyi Fagade akizungumza na waandishi wa habari jana walipotembelea moja ya mradi wa uhifadhi wa mazingira katika Kata ya Mpamantwa, wilayani Bahi. Fagade alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huu katika kulinda mazingira na kuhakikisha mustakabali endelevu.

Alisisitiza umuhimu wa utulivu wa mazingira katika kusaidia mfumo wa ikolojia na viumbe hai, pia umuhimu wa kushirikiana na Lead Foundation. "Mazingira ni muhimu kwetu, bila ya uhifadhi wake, shughuli zetu na jumuiya tunazohudumia zingeweza kuathirika. Ushirikiano huu na Lead Foundation, hasa kupitia mradi wake wa urejeshaji wa miti ya Kisiki Hai, unahusisha mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara na Arusha,” alisema Fagade.


Lilian Pascal, Meneja Biashara na Masoko wa Kampuni hiyo, aliunga mkono maoni ya Fagade, akiangazia jukumu muhimu la ulinzi wa mazingira katika kupambana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa. "Ahadi yetu ya utunzaji wa mazingira inawiana na wajibu wetu kwa wateja wetu na jamii. Uzalishaji wa bidhaa za Heineken unategemea sana maji, hivyo basi ni muhimu kwetu kuweka kipaumbele katika uhifadhi wa mazingira," Lilian alisema.

Mkurugenzi wa Miradi wa Taasisi ya Lead Foundation, Njamasi Chiwanga akitoa maelezo kuhusu mipango inayoendelea inayolenga ufufuaji wa misitu na uvunaji wa maji ya mvua. Mradi wa 'Kisiki Hai' unaolenga kuotesha miti, tayari umepiga hatua kubwa na kufikia zaidi ya vijiji 500 katika mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara na Arusha. “Hadi sasa mradi wetu umefanikiwa kulima miti zaidi ya milioni 18 na kushirikisha wananchi zaidi ya 200,000,” Chiwanga alibainisha.


Mkazi wa eneo hilo Bosco Malogo alielezea kufurahishwa na athari chanya za mradi huo kwa jamii yao. Kupitia mbinu bunifu kama vile kupanda miti kutoka kwa vishina vilivyo hai, wakazi wameshuhudia manufaa yanayoonekana ikiwa ni pamoja na malisho ya mifugo, matunda ya dawa, na uanzishwaji wa haraka wa misitu kwa gharama ndogo. "Mradi huu umebadilisha mazingira yetu, kutoa suluhu endelevu ambazo zinanufaisha watu na asili," alibainisha Malogo.


Heineken Tanzania bado imejitolea kuendeleza uendelevu wa mazingira na kuunga mkono mipango inayokuza ustawi wa jamii kote Tanzania.




Mkurugenzi mkazi wa Kampuni ya Heineken Tanzania, Obabiyi Fagade akishirikiana na wananchi wa Kijiji cha Mpamantwa, wilayani Bahi, Dodoma kuokoa miti iliyokatwa.




MAASKOFU wa Kanisa la Anglikana wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 11-5-2024, wakiwa Zanzibar kwa ajili ya Ibada ya Maridhiano kutokana na madhila waliyofanyiwa Waafrika wakati wa Biashara ya Utumwa inayotarajiwa kufanyika kesho 12-5-2024 katika Kanisa la Anglikana Mkunazini Jijini Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Askofu Mkuu Mhashamu Justin Welby,mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 11-5-2024, akiwa na Ujumbe wake, wakiwa Zanzibar kwa ajili ya Ibada ya Maridhiano kutokana na madhila waliyofanyiwa Waafrika wakati wa Biashara ya Utumwa inayotarajiwa kufanyika kesho 12-5-2024 katika Kanisa la Anglikana Mkunazini Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba mkoani Dodoma tarehe 11 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa hafla ya kufungua Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba na Kukabidhi Magari 21 kwa Jeshi la Polisi iliyofanyika eneo la Mtumba Mkoani Dodoma  tarehe 11 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua Gwaride la Jeshi la Polisi mara baada ya kuwasili eneo la Mtumba Mkoani Dodoma kufungua Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba na Kukabidhi Magari 21 kwa Jeshi la Polisi. Tarehe 11 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka jiwe la msingi la Ufunguzi wa Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba mkoani Dodoma tarehe 11 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kuhusu mfumo wa kidijitali wa ufunguaji kesi uliopo katika Kituo cha Polisi Mtumba wakati wa akikagua kituo hicho katika hafla ya  Ufunguzi wa Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba mkoani Dodoma tarehe 11 Mei 2024.



 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kufuata taratibu, kuzingatia sheria ya Jeshi la Polisi na kanuni za Polisi katika kufanya kazi za Kipolisi ikiwemo kukamata, kufanya upekuzi, kushikilia, kupeleleza watuhumiwa pamoja na kuwahoji mashahidi na watuhumiwa.


Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa hafla ya kufungua Kituo cha Polisi Daraja “A” Wilaya ya Kipolisi Mtumba na Kukabidhi Magari 21 kwa Jeshi la Polisi, hafla iliyofanyika eneo la Mtumba Mkoani Dodoma. Amesema Maadili mema, nidhamu kazini na uwajibikaji ni nguzo muhimu kwa Jeshi la Polisi katika kusimamia sheria. Makamu wa Rais amelipongeza Jeshi la Polisi pamoja na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kuimarisha Amani na usalama hapa nchini.


Aidha Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kubadilika kwa haraka ili kuweza kukabiliana na mbinu mpya za uhalifu kwa kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake. Amewasihi kujielekeza zaidi katika kubuni na kutumia mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha Askari na Makamanda wanapata mafunzo ya mara kwa mara kwenye maeneo ya intelijensia, usalama na uhalifu wa kimtandao,akili mnemba na matumizi ya roboti pamoja na kuunganisha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Mikoa, Wilaya, Vikosi, Vitengo na Vituo vyote vya Polisi nchini ili kurahisisha mawasiliano.


Vilevile Makamu wa Rais amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuangalia upya mfumo mzima wa utoaji leseni, ukaguzi wa magari, matumizi ya teknolojia hususan kamera za barabarani na matumizi ya Body-cam jackets  zitakazoonesha mazungumzo baina ya askari na madereva ili kudhibiti rushwa barabarani,kuimarisha weledi na uthabiti wa vyombo vya moto hali itakayosaidia katika kudhibiti ajali za barabarani.


Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kujenga uhusiano mzuri kati yake na wananchi ili liweze kufanikiwa kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu wa aina zote. Pia ameitaka jamii kuheshimu sheria na taratibu za Jeshi la Polisi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. Amesema Jitihada zinazofanyika kupitia dhana ya Polisi Jamii ni budi ziendelezwe.


Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai yaliyo ndani ya uwezo wake  ikiwemo kuimarisha Madawati ya Malalamiko ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi kwa kuyapatia watumishi wa kutosha wenye weledi kwenye masuala ya uchunguzi ili kuendelea kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi nchini.


Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amesema Jeshi la Polisi limeendelea kukuza matumizi mbalimbali ya mifumo ya TEHAMA ikiwa ni utekelezaji maelekezo ya Mheshimiwa Rais katika kuleta ufanisi, uwazi na uharaka wa kazi za Kipolisi kwa lengo la kuharakisha masuala yote ya haki jinai na kuhakikisha yanatendeka kwa tija.


Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura amesema Jeshi la Polisi linatambua deni kubwa walilonalo kwa Serikali na Wananchi hivyo litazidisha utendaji wenye nidhamu ya hali ya juu, haki, uadilifu na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi ni huduma sahihi na zinazotakiwa. 


Ameongeza kwamba ujenzi wa Vituo hivyo vya kisasa vya Polisi utawezesha kutafsiri madhumuni halisi ya kuwepo kwa Jeshi la Polisi kwa kuwa majengo hayo ni rafiki hata kwa watendaji katika kutimiza wajibu wao.  


Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

11 Mei 2024

Dodoma.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika mazungumzo na Ujumbe wa Wabunge kutoka Nchini Korea Kusini, ukiongozwa na Mhe. Sul Hoon (kulia kwa Rais) mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 11-5-2024.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na wageni wake Ujumbe wa Wabunge kutoka Nchini Korea Kusini, ukiongozwa na Mhe. Sul Hoon (kulia kwa Rais) mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 11-5-2024.
(Picha na Ikulu)

Top News